Jeremiah 4


1 a“Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli,
nirudie mimi,”
asema Bwana.
“Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu
na usiendelee kutangatanga,

2 bikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa,
‘Kwa hakika kama vile Bwana aishivyo,’
ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye
na katika yeye watajitukuza.”

3 cHili ndilo asemalo Bwana kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu: “Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu,
wala msipande katikati ya miiba.

4 dJitahirini katika Bwana,
tahirini mioyo yenu,
enyi wanaume wa Yuda
na watu wa Yerusalemu,
la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu
na kuwaka kama moto
kwa sababu ya uovu mliotenda,
ikiwaka pasipo wa kuizima.

Maafa Kutoka Kaskazini


5 “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu na kusema:
‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’
Piga kelele na kusema:
‘Kusanyikeni pamoja!
Tukimbilie katika miji yenye maboma!’

6 eOnyesheni ishara ili kwenda Sayuni!
Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa!
Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini,
maangamizi ya kutisha.”


7 fSimba ametoka nje ya pango lake,
mharabu wa mataifa amejipanga.
Ametoka mahali pake
ili aangamize nchi yenu.
Miji yenu itakuwa magofu
pasipo mtu wa kuishi humo.

8 gHivyo vaeni nguo za magunia,
ombolezeni na kulia kwa huzuni,
kwa kuwa hasira kali ya Bwana
haijaondolewa kwetu.


9 “Katika siku ile,” asema Bwana
“mfalme na maafisa watakata tamaa,
makuhani watafadhaika,
na manabii watashangazwa mno.”

10 hNdipo niliposema, “Aa, Bwana Mwenyezi, umewadanganyaje kabisa watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kwenye koo zetu!”

11 iWakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame katika jangwa unavuma kuelekea watu wangu, lakini sio kupepeta au kutakasa, 12 jupepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”
13 kTazama! Anakuja kama mawingu,
magari yake yanakuja kama upepo wa kisulisuli,
farasi wake wana mbio kuliko tai.
Ole wetu! Tunaangamia!

14 lEe Yerusalemu, usafishe uovu kutoka moyoni mwako na uokolewe.
Utaendelea kuficha mawazo mapotovu mpaka lini?

15 mSauti inatangaza kutoka Dani,
ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.

16 “Waambie mataifa jambo hili,
piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu:
‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali,
likipiga kelele ya vita dhidi ya miji ya Yuda.

17 nWamemzunguka kama watu walindao shamba,
kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ”
asema Bwana.

18 o“Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe
yameleta haya juu yako.
Hii ndiyo adhabu yako.
Tazama jinsi ilivyo chungu!
Tazama jinsi inavyochoma moyo!”


19 pEe mtima wangu, mtima wangu!
Ninagaagaa kwa maumivu.
Ee maumivu makuu ya moyo wangu!
Moyo wangu umefadhaika ndani yangu,
siwezi kunyamaza.
Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta,
nimesikia kelele ya vita.

20 qMaafa baada ya maafa,
nchi yote imekuwa magofu.
Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa,
makazi yangu kwa muda mfupi.

21 rHata lini nitaendelea kuona bendera ya vita
na kusikia sauti za tarumbeta?


22 s“Watu wangu ni wapumbavu,
hawanijui mimi.
Ni watoto wasio na akili,
hawana ufahamu.
Ni hodari kutenda mabaya,
hawajui kutenda yaliyo mema.”


23 tNiliitazama dunia,
nayo haikuwa na umbo tena ni tupu;
niliziangalia mbingu,
mianga ilikuwa imetoweka.

24 uNiliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka,
vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.

25 vNilitazama, wala watu hawakuwepo;
kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.

26 Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa,
miji yake yote ilikuwa magofu
mbele za Bwana,
mbele ya hasira yake kali.

27 wHivi ndivyo Bwana asemavyo:
“Nchi yote itaharibiwa,
ingawa sitaiangamiza kabisa.

28 xKwa hiyo dunia itaomboleza
na mbingu zilizo juu zitakuwa giza,
kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma,
nimeamua na wala sitageuka.”


29 yKwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde
kila mji unakimbia.
Baadhi wanakimbilia vichakani,
baadhi wanapanda juu ya miamba.
Miji yote imeachwa,
hakuna aishiye ndani yake.


30 zUnafanya nini, ewe uliyeharibiwa?
Kwa nini unajivika vazi jekundu
na kuvaa vito vya dhahabu?
Kwa nini unapaka macho yako rangi?
Unajipamba bure.
Wapenzi wako wanakudharau,
wanautafuta uhai wako.


31 aaNasikia kilio kama cha mwanamke
katika utungu wa kuzaa,
kilio cha uchungu kama cha anayemzaa
mtoto wake wa kwanza:
kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua,
akiinua mikono yake, akisema,
“Ole wangu! Ninazimia;
maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”
Copyright information for SwhKC